Viongozi wa Kiislamu Uasin Gishu Wataka Mageuzi ya Haraka Usalama wa Ndani, Waonya Machafuko 2027
“Wakati huu shule zinajiandaa kufunguliwa, tunahofia usalama wa watoto wetu iwapo mikutano ya kisiasa itaendelea kushuhudia vita na machafuko kama yale tuliyoyaona katika Kaunti ya Homa Bay”
Viongozi wa Kiislamu, wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini,wakihutubia wanahabari jijini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, kuhusu ongezeko la uchochezi wa kisiasa, lugha ya chuki na usalama wa taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
By James Gitaka
Viongozi wa Kiislamu katika Kaunti ya Uasin Gishu sasa wanataka kufanyiwa mabadiliko ya haraka katika Wizara ya Usalama wa Ndani na taasisi nyingine za serikali zinazohusika na ulinzi wa wananchi, wakisema kuna udhaifu mkubwa katika kukabiliana na uchochezi wa kisiasa, lugha ya chuki na machafuko yanayoshuhudiwa katika baadhi ya mikutano ya kisiasa nchini.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK) Kanda ya North Rift, Sheikh Abubakar Bini, pamoja na viongozi wengine wa Kiislamu Mohammed Ali na Abdulkadir Mohammed, viongozi hao wameonya kuwa taifa linaweza kuelekea katika machafuko makubwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa dhidi ya viongozi na watu wanaotuhumiwa kueneza chuki na uchochezi wa kisiasa.
Viongozi hao wameeleza masikitiko yao kwamba baadhi ya watu waliotakiwa kufika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) wameendelea kupuuza wito huo, licha ya madai kwamba wamehusishwa na matamshi yanayoweza kuchochea migawanyiko na kuhatarisha amani ya taifa.
Sheikh Bini alisema hali hiyo inatia wasiwasi mkubwa, hasa wakati taifa linapoendelea kushuhudia matukio ya vurugu katika baadhi ya maeneo yanayohusishwa na shughuli za kisiasa.
“Tunasikitika kuona kwamba kati ya wale waliotakiwa kujifikisha mbele ya tume ya NCIC, wengine wanapuuza wito huo, ilhali wamebainika kuwa na lugha za chuki ambazo zinaweza kupeleka taifa letu katika machafuko,” alisema Sheikh Bini.
Kiongozi huyo wa Kiislamu alisema kuna haja ya taasisi zinazohusika kuhakikisha uwajibikaji wa viongozi wote wanaotoa matamshi ya uchochezi, bila kuzingatia misimamo ya kisiasa, umaarufu au nafasi zao katika jamii.
Bini pia alieleza wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wakati shule zikitarajiwa kufunguliwa, akisema kuendelea kwa vurugu katika mikutano ya kisiasa kunaweza kuhatarisha maisha na shughuli za kawaida za wananchi.
“Wakati huu shule zinajiandaa kufunguliwa, tunahofia usalama wa watoto wetu iwapo mikutano ya kisiasa itaendelea kushuhudia vita na machafuko kama yale tuliyoyaona katika Kaunti ya Homa Bay na maeneo mengine nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Abdulkadir Mohammed alisema matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo yanaibua maswali mazito kuhusu utayari na uwezo wa Wizara ya Usalama wa Ndani pamoja na taasisi nyingine za serikali kutekeleza jukumu lao la kulinda wananchi na mali zao.
Alidai kuwa kufungwa kwa baadhi ya barabara na kutokea kwa machafuko kulipaswa kuzuiwa kabla hali haijaharibika.
“Hii ni ishara kwamba wizara na taasisi za serikali zilizopewa jukumu la kuhakikisha usalama wa Wakenya zimelala. Wakati barabara zikifungwa na vijana wakisababisha machafuko, taasisi za usalama zilikuwa wapi? Hasa Homa Bay na maeneo mengine, hatua zingechukuliwa mapema kuzuia hali hiyo,” alisema Abdulkadir.
Mohammed alitaka kufanywe mabadiliko katika baadhi ya taasisi za usalama ili kurejesha imani ya wananchi, akisema viongozi waliopo wanapaswa kuwajibishwa iwapo wanashindwa kutekeleza majukumu waliyopewa.
“Tunaomba kuwepo na mabadiliko katika taasisi hizo kwa sababu waliopo kwa sasa wameonekana kushindwa kuwahakikishia Wakenya usalama wao na mali zao,” aliongeza.
Naye Mohammed Ali alionya kuwa kuendelea kwa vurugu za kisiasa na kile alichokitaja kuwa kutotekelezwa kwa sheria kwa usawa kunaweza kusababisha Wakenya kupoteza kabisa imani katika taasisi za serikali, hususan vyombo vya usalama.
Ali alisema imani ya wananchi katika serikali na taasisi zake ni muhimu katika kudumisha utulivu wa taifa, akisisitiza kuwa mamlaka zinapaswa kuchukua hatua sawa dhidi ya kila mtu anayekiuka sheria bila kujali upande wa kisiasa anaounga mkono.
“Iwapo visa hivi vitaendelea, Wakenya watakosa imani kabisa na taasisi za serikali, na hasa idara za usalama. Sheria lazima itekelezwe kwa usawa na kila mtu anayehusishwa na uchochezi au lugha ya chuki awajibishwe,” alisema Ali.
Kiongozi huyo pia ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuiga mfano wa Kanisa Katoliki katika msimamo wake dhidi ya kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa.
Ali alisema viongozi wa kidini wana wajibu wa kuhakikisha nyumba za ibada zinabaki kuwa maeneo ya kuhubiri amani, umoja na maadili, badala ya kutumiwa na wanasiasa wanaotuhumiwa kueneza chuki na mgawanyiko.
“Tunatoa wito kwa viongozi wote wa dini kuiga mfano wa Kanisa Katoliki. Kanisa limechukua msimamo wa kutowapa majukwaa wanasiasa ambao wengi wao wameonekana kutumia lugha inayoweza kueneza chuki na mgawanyiko,” alisema.
Ali alionya kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kukumbuka kuwa uchaguzi ni tukio la muda, lakini taifa na wananchi wataendelea kuishi pamoja hata baada ya uchaguzi mkuu.
“Taifa hili litakuwepo hata baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Ni lazima amani, umoja na uwiano wa kitaifa viendelee kuimarishwa. Tusikubali siasa za uchaguzi kutugawanya na kuharibu amani ambayo Wakenya wameijenga kwa miaka mingi,” alionya.
Viongozi hao sasa wanataka NCIC, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Polisi na taasisi nyingine zenye jukumu la kulinda usalama wa taifa kuchukua hatua bila upendeleo dhidi ya wote wanaotuhumiwa kueneza lugha ya chuki au kuchochea machafuko.
Wamesisitiza kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kurejesha imani ya wananchi katika taasisi za serikali na kuhakikisha taifa linaingia katika kipindi cha uchaguzi ujao likiwa na mazingira ya amani, usalama na uwiano wa kitaifa.
