SHUGHULI YA TOHARA YA VIJANA YAZUA TASHWISHI KUFUATIA TANGAZO LA WAZEE
Tangazo hilo, lililotolewa kwa kuzingatia maslahi ya vijana, limetokana na sababu kwamba vijana hao wanatarajiwa kujiunga na gredi ya tisa mwaka ujao
By Calvin Chitwa
Tashwishi imezuka kuhusu shughuli ya tohara ya vijana kote nchini mwezi huu wa Desemba kufuatia tangazo la baadhi ya wazee wa kijamii wakitaka shughuli hizo ziahirishwe hadi mwaka ujao.
Tangazo hilo, lililotolewa kwa kuzingatia maslahi ya vijana, limetokana na sababu kwamba vijana hao wanatarajiwa kujiunga na gredi ya tisa mwaka ujao. Hivyo basi, wazee hao wanaona kuwa hawapaswi kujiunga na wenzao ambao bado hawajapata mafunzo maalum yanayotolewa wakati wa kupashwa tohara.
Hata hivyo, hali hiyo imeibua changamoto, huku vituo vya makanisa vinavyotoa huduma hizo kila mwaka vikishuhudia kupungua kwa idadi ya vijana wanaoshiriki.
Viongozi wa kidini wakiongozwa na Kasisi William Gituku wa Kanisa la PCEA Ayub Kinyua, Eldoret, ambao wanasimamia vituo hivyo, wamesema kwamba hawapingi tangazo hilo. Hata hivyo, wamewaonya wazazi dhidi ya kuwapeleka watoto wao katika maeneo yasiyoidhinishwa ili kuepuka hatari na maafa wakati wa shughuli hiyo.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa madaktari waliobobea wanashiriki katika shughuli hii ili kuepusha kuhatarisha maisha ya vijana,” alisisitiza Kasisi Gituku.
Aidha, viongozi hao walitoa wito wa kuzingatia usafi wa hali ya juu na kutoa mafunzo bora yanayolenga kuwaandaa vijana kwa maisha yao ya baadaye, bila kuwadhuru kisaikolojia au kijamii.