Na Judith Waka
Catherine ni mfanyabiashara wa simu anayefanya biashara yake katika mji wa Eldoret. Baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu, alitarajia kupata ajira na kujenga maisha mazuri. Hata hivyo, licha ya juhudi zake za kutafuta kazi, hakuweza kupata ajira baada ya kumaliza masomo.
“Nilikuwa na tarajio la kupata kazi baada ya masomo yangu, lakini kwa sababu sikupata hio fursa, ikabidi nitafte jinsi ya kupata hela kwa kupitia hii kazi ambayo nafanya.
Kwa sababu ya hitaji la kujipatia kipato, Catherine aliamua kuingia katika biashara ya kuuza simu badala ya kukaa nyumbani bila kufanya chochote. Biashara hii imempa nafasi ya kupata kipato, ingawa anakabiliwa na changamoto mbalimbali.  Moja ya changamoto kubwa anayokumbana nayo ni ukosefu wa mtaji wa kutosha wa kuendesha na kukuza biashara yake. Pia, hukutana na wateja ambao hawana pesa za kutosha kununua simu. Wakati mwingine, hali hii humfanya kupata hasara pale wateja wanaposhindwa kulipa kiasi kamili cha pesa wanachodaiwa.
” Nauza simu ya lipa mdogo mdogo, wateja wanataka simu lakini hawana hela ya kutosha ya kununua. Changamoto kuu ambacho nachokipitia ni kukosa hela.”
Licha ya changamoto hizo, Catherine anaendelea kujituma. Anasema ni afadhali aje mjini kutafuta pesa, hata kama ni kidogo, kuliko kukaa nyumbani bila kufanya chochote. Kwake, kila kiasi cha pesa anachopata ni muhimu katika kukidhi mahitaji yake ya kila siku.  Catherine anaamini kuwa serikali inapaswa kuunda nafasi zaidi za ajira kwa vijana kama yeye. Anaamini kuwa fursa zaidi za ajira zingewawezesha vijana kutumia ujuzi na elimu yao kujenga maisha bora.  Licha ya changamoto anazokutana nazo, Catherine anasema kinachompa furaha zaidi ni kuwa na afya njema na kuweza kupata pesa, hata kama ni kidogo. Pia, anajivunia kuwa mkenya, hasa kwa sababu anathamini amani iliyopo nchini.  Hadithi ya Catherine inaonyesha juhudi na azma ya vijana wengi ambao, licha ya changamoto ya ukosefu wa ajira rasmi, wanaendelea kujitafutia fursa na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga maisha bora ya baadaye.