WAZEE WA BAJUNI UASIN GISHU WALAANI OPERESHENI YA USALAMA SIYU, LAMU

0

“Wananchi wa Lamu wanahitaji amani na maendeleo sawa na Wakenya wengine. Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa kweli wakati jamii zetu bado zinakabiliwa na hofu, vizuizi vya usafiri na changamoto za kiuchumi zinazotokana na mazingira ya muda mrefu ya kiusalama,” alisema Abdulaziz Mohammed.

Sheikh Abubakar Bini Mwenyekiti wazee wa Bajuni kaunti ya Uasin Gishu

Na James Gitaka

Wazee wa jamii ya Bajuni wanaoishi Kaunti ya Uasin Gishu wamejitokeza kulaani vikali operesheni ya usalama iliyotekelezwa katika kijiji cha Siyu, Kisiwa cha Pate, Kaunti ya Lamu, wakidai kuwa mazingira yaliyoizunguka yamezua maswali kuhusu uhalali wake na uzingatiaji wa taratibu za kisheria.

Wakizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Madaraka, wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti wao, Sheikh Abubakar Bini, walisema kuna haja ya serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu operesheni hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia leo. Kulingana na Sheikh Bini, wananchi wanastahili kufahamishwa kuhusu sababu, malengo na mamlaka yaliyoruhusu hatua hiyo.

“Tunaiomba serikali kueleza wazi kilichotokea Siyu. Wananchi wana haki ya kujua iwapo taratibu zote za kikatiba na kisheria zilifuatwa kabla ya operesheni hiyo kufanyika. Hatujaona tangazo rasmi wala mjadala wowote uliofanyika katika vyombo husika kuhusu hatua kama hiyo,” alisema Sheikh Bini.

Kauli hiyo inajiri huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiendelea kushinikiza uchunguzi huru kufuatia madai ya wakazi wa Siyu kwamba watu waliovalia sare za kijeshi walivamia makazi yao alfajiri na kuwafanyia ukatili. Mashirika ya MUHURI na Haki Africa yameeleza wasiwasi kuhusu madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia katika eneo hilo. Aidha, viongozi mbalimbali wa pwani wameitaka Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.

Wazee hao walisisitiza kuwa licha ya taifa kuadhimisha miaka ya kujitawala kupitia Siku ya Madaraka, wakazi wa Lamu bado wanaendelea kuathiriwa na changamoto za kiusalama na kiuchumi ambazo zimeendelea kwa muda mrefu. Walisema hatua mbalimbali za kiusalama zilizowekwa kwa miaka mingi zimeathiri biashara, usafiri na uwekezaji katika eneo hilo.

“Wananchi wa Lamu wanahitaji amani na maendeleo sawa na Wakenya wengine. Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa kweli wakati jamii zetu bado zinakabiliwa na hofu, vizuizi vya usafiri na changamoto za kiuchumi zinazotokana na mazingira ya muda mrefu ya kiusalama,” alisema Abdulaziz Mohammed.

Wazee hao pia walirejelea amri ya muda mrefu iliyokuwa ikizuia safari za usiku katika barabara kuu zinazoingia Kaunti ya Lamu, wakisema hatua hiyo imeathiri uchumi wa eneo hilo kwa miaka mingi. Hivi karibuni, Mahakama Kuu ya Garsen ilitoa amri za muda kusitisha utekelezaji wa masharti hayo huku kesi inayopinga uhalali wake ikiendelea kusikilizwa, ingawa wakazi wamekuwa wakilalamikia kile wanachodai kuwa ni kuendelea kwa baadhi ya vizuizi licha ya uamuzi wa mahakama.

Hata hivyo, serikali imekuwa ikitetea operesheni mbalimbali za kiusalama katika eneo la Lamu chini ya Operesheni Amani Boni, ikisema zimechangia kupunguza vitisho vya ugaidi na kulinda miradi muhimu ya kitaifa ikiwemo ukanda wa maendeleo wa LAPSSET na miundombinu ya bandari ya Lamu. Maafisa wa usalama wamekuwa wakisisitiza kuwa operesheni hizo ni muhimu katika kudhibiti makundi ya kigaidi yanayovuka mpaka wa Kenya na Somalia.

Wazee wa Bajuni sasa wanaitaka serikali kuhakikisha kuwa hatua zote za kiusalama zinafanyika kwa kuzingatia haki za binadamu, sheria za nchi na ushirikishwaji wa wananchi ili kuimarisha imani kati ya jamii na vyombo vya usalama.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *