Viongozi wa Kiislamu Waonya: ‘Serikali Isikize Vijana au Itarajie Ghasia’

0

“Tumewasikia vijana wetu wakitoa kauli zinazoashiria kupoteza imani na uongozi wa Rais William Ruto.Badala ya kuzibeza, ni muhimu vijana wapate sikio” Sheikh Bini

Viongozi wa Kiislamu nje ya Msikiti wa Masjid Nur Eldoret.

Viongozi wa Kiislamu kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa wamewataka wanasiasa kujadili kwa kina malalamiko ya vijana wa taifa, ambao mara kwa mara wamekuwa wakieleza waziwazi kutoridhishwa kwao na uongozi wa Rais William Ruto.

Sheikh Abubakar Bini: Vijana Wapate Sikio

Wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini, Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Dini ya Kiislamu, viongozi hao walizungumza baada ya kushiriki ibada ya maombi kuashiria kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, iliyofanyika katika Msikiti wa Masjid Nur.

“Tumewasikia vijana wetu wakitoa kauli zinazoashiria kupoteza imani na uongozi wa Rais William Ruto. Ingawa baadhi ya kauli hizi zimekosolewa na viongozi wa kisiasa na maafisa wa usalama, badala ya kuzibeza, ni muhimu vijana wapate sikio ili kuhakikisha matakwa yao yanashughulikiwa na serikali kwa ajili ya kudumisha utulivu nchini,” alisema Sheikh Bini.

Lawama kwa Wabunge Kuhusu Nyongeza ya Mishahara

Aidha, viongozi hao wa Kiislamu waliwalaumu wabunge kwa kuidhinisha nyongeza ya mishahara yao, hatua iliyotangazwa na Tume ya Kuratibu Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC), ambayo itawagharimu wananchi zaidi ya shilingi bilioni nne.

“Masuala kama haya ya wabunge kujiongezea mishahara minono wakati Wakenya wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya uchumi, shule zikikosa ufadhili wa serikali kwa wakati, na huduma za umma zikidorora, ndiyo yamekuwa yakilalamikiwa na vijana kwenye maandamano ya Gen Z. Wabunge wanapaswa kukataa nyongeza hii, la sivyo hata sisi viongozi wa kidini tutaungana na vijana kukashifu serikali,” aliongeza Sheikh Bini.

Wito wa Kuondoa Tofauti Katika Siku Kuu za Kiislamu

Kwa upande wake, Jamal Diriwo, mmoja wa viongozi wa vijana wa Kiislamu katika eneo la North Rift, alitoa wito kwa viongozi wa Kiislamu na maulamaa nchini kubuni kamati ya mashauriano na kushirikiana na Kadhi Mkuu ili kuweka mwongozo wa kutangaza siku rasmi za matukio muhimu ya Kiislamu.

“Inashangaza kuona Waislamu wakisherehekea mwisho wa Ramadhani kwa tarehe tofauti kila mwaka. Tofauti hizi zinaweza kuepukwa iwapo kutakuwepo na mashauriano kati ya viongozi wa Kiislamu, mashirika ya Kiislamu, na Kadhi Mkuu wetu,” alisisitiza Diriwo.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *