Viongozi wa Kiislamu North Rift Wataka Umoja wa Ramadhani na Idd

0

“Huu si tu mjadala wa tarehe, bali ni suala la kulinda utamaduni na mshikamano wa Waislamu”

Abubakar Bini. Photo/Achieng Kemuma

Viongozi wa Kiislamu kutoka ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa wamewataka wanavyuoni pamoja na maimamu nchini kutafuta mwafaka wa pamoja utakaowawezesha Waislamu kushiriki kwa umoja ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea sikukuu ya Idd kwa wakati mmoja.

Wakizungumza mjini Eldoret, wakiongozwa na Imamu wa AP Masjid, Sheikh Abdulaziz Mohammed, viongozi hao walieleza kuwa tofauti za tarehe za kuanza na kumaliza Ramadhani zimekuwa zikigawa jamii ya Kiislamu, hali ambayo wanasema inahitaji suluhu ya haraka.

“Ni muhimu kwa wanavyuoni wetu kukaa pamoja na kukubaliana juu ya mwongozo mmoja wa kuandama mwezi ili Waislamu wote nchini washiriki ibada na sherehe kwa pamoja,” alisema Sheikh Abdulaziz Mohammed.

Aliongeza kuwa katika miaka ya awali, Waislamu kote nchini walikuwa wakisherehekea Idd kwa pamoja, jambo lililodumisha mshikamano wa kijamii na kuimarisha maadili ya kidini.

“Zamani, sherehe za Idd zilikuwa za pamoja na zilijenga umoja mkubwa. Watoto walifurahia kupokea ‘mkono wa Idd’ kutoka kwa jamaa na marafiki, lakini sasa mila hii imeanza kupotea kutokana na mgawanyiko huu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Kanda ya North Rift, Sheikh Abubakar Bini, alisisitiza kuwa tofauti hizo zinaweza kuepukika iwapo kutakuwa na ufuataji wa mwongozo wa pamoja wa kitaaluma kuhusu kuandama kwa mwezi.

“Ikiwa tutafuata mwafaka wa wanavyuoni kuhusu kuonekana kwa mwezi, basi tutakuwa na umoja si tu nchini Kenya bali hata katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Sheikh Bini.

Alibainisha kuwa umoja huo utasaidia kuhifadhi mila muhimu za Kiislamu kama vile utoaji wa ‘mkono wa Idd’, ambao kwa miaka mingi umekuwa ukileta furaha kwa watoto wengi wa Kiislamu.

“Huu si tu mjadala wa tarehe, bali ni suala la kulinda utamaduni na mshikamano wa Waislamu wetu,” aliongeza.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na tofauti miongoni mwa Waislamu nchini kuhusu tarehe za kuanza na kumaliza mwezi wa Ramadhani pamoja na kusherehekea Idd, kutokana na mbinu tofauti za kuthibitisha kuonekana kwa mwezi. Hali hii imepelekea baadhi ya jamii kusherehekea sikukuu hizi kwa nyakati tofauti, jambo linalodhoofisha umoja wa waumini na kuathiri baadhi ya mila za kijamii zilizokuwepo kwa muda mrefu.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *