Mgogoro wa SUPKEM wazidi kuchacha: Wito wa uwajibikaji na uchaguzi mpya
“Fedha za mahujaji ni amana takatifu. Viongozi wa SUPKEM wanapaswa kutoa maelezo ya kina na kuonyesha wazi jinsi fedha hizo zilitumika,”Mbunge wa Fafi, Salah Yakub,
Waislamu Wazidi Kushinikiza mageuzi Ndani ya SUPKEM/ Hubzmedia
Vijana wa Kiislamu kutoka eneo la Bonde la Ufa wamewasilisha ombi kwa Kamati ya Bunge la Kitaifa inayochunguza migogoro ya Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (SUPKEM), wakitaka uongozi wa sasa wa baraza hilo unaoongozwa na Hassan Ole Naado kusimamishwa mara moja hadi uchunguzi wa tuhuma dhidi yao utakapo kamilika.
Wakiongozwa na Sheikh Jamal Diriwo na mwanachama wa CIPK Kanda ya Rift Valley Sheikh Abubakar Kisaka, viongozi hao wametilia shaka barua iliyotolewa na SUPKEM hapo jana kuhusu maandalizi ya Hija ya mwaka 2026. Wamesema maandalizi ya Hija ndiyo mojawapo ya masuala yanayochunguzwa na Kamati ya Bunge, hususan kuhusu matumizi mabaya ya fedha na kuondolewa kwa baadhi ya mawakala kinyume cha sheria.
“Tunataka maandalizi ya Hija ya mwaka 2026 yasitishwe mara moja hadi ukweli ujulikane. Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu na haitakiwi kufunikwa na ufisadi na ukosefu wa uwajibikaji,” alisema Sheikh Abubakar Kisaka.
Wito wa mageuzi ya Katiba ya SUPKEM
Waislamu hao wamesema tayari wameanzisha mchakato wa ukusanyaji saini ili kumuondoa Ole Naado madarakani. Aidha, wametaka mabadiliko makubwa ya Katiba ya SUPKEM ili kuhakikisha viongozi watakaochaguliwa kuongoza baraza hilo wanakuwa na kiwango cha elimu kinachohitajika na maadili bora.
Mgogoro wa muda mrefu
Mgogoro ndani ya SUPKEM si mpya. Kwa muda mrefu, Waislamu wengi wameelezea kutokuwa na imani na uongozi wa sasa, jambo lililopelekea kuundwa kwa Kamati ya Bunge kuchunguza malalamiko dhidi ya Hassan Ole Naado.
Mbunge wa Fafi, Salah Yakub, pia ameungana na waumini wanaotaka uwajibikaji, akisisitiza kuwa madai ya ufujaji wa fedha za Hija hayawezi kupuuzwa.
“Fedha za mahujaji ni amana takatifu. Viongozi wa SUPKEM wanapaswa kutoa maelezo ya kina na kuonyesha wazi jinsi fedha hizo zilitumika,” alisema Yakub.
Malalamiko ya mahujaji na mawakala
Katika Hija ya mwaka huu, baadhi ya mahujaji na mawakala walilalamikia changamoto za malazi duni, uhaba wa vyoo na gharama za juu za ada za usimamizi zilizoongezwa kutoka dola 20 hadi dola 100 za Kimarekani. Walisema hali hiyo ilidhihirisha ukosefu wa maandalizi na usimamizi bora kutoka kwa SUPKEM.
Jibu la SUPKEM
Hata hivyo, Mwenyekiti wa SUPKEM, Hassan Ole Naado, ametetea uongozi wake akisema barua na taarifa zinazozunguka mitandaoni hazina msingi. Ameeleza kuwa Katiba ya baraza hilo inatoa muda wa miaka mitano kwa mwenyekiti, hivyo hakuna uvunjaji wa sheria katika uongozi wake.
“Hakuna mgogoro wa kikatiba. Uongozi wa SUPKEM upo imara na tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria,” alisema Ole Naado.
Mgogoro wa SUPKEM unaendelea kuzua taharuki miongoni mwa Waislamu nchini, huku vijana, viongozi wa kidini na wanasiasa wakisisitiza haja ya uwazi, uwajibikaji na uchaguzi mpya wa viongozi. Hali hii imeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa usimamizi wa ibada ya Hija na uongozi wa juu wa Waislamu nchini Kenya.
