Maimamu wa North Rift Waongoza Maombi ya Taifa, Watoa Wito wa Hatua Dhidi ya Changamoto Zinazoikabili Kenya

0

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu alete mvua ya  baraka na kuisaidia nchi yetu. Taifa linapitia kipindi kigumu kinachohitaji umoja, hekima na hatua za pamoja kutoka kwa kila upande,”

Viongozi wa dini wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini, Rajab Kipkorir Salah na Azizi Ndamwe Wakoli wakizungumza na wanahabari baada ya maombi ya kuliombea taifa. Walitoa wito wa umoja na hatua dhidi ya changamoto zinazolikabili Kenya.

Maimamu kutoka eneo la North Rift wameungana katika maombi maalum ya kuliombea taifa, huku wakitoa wito wa hatua za haraka kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, ikiwemo ukosefu wa mvua inayotishia uzalishaji wa chakula na maisha ya mamilioni ya Wakenya.

Maombi hayo yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Dini ya Kiislamu North Rift, Sheikh Abubakar Bini, yalilenga kuiombea Kenya amani, umoja na kupata suluhu kwa matatizo yanayoikumba nchi.

Sheikh Bini amesema ukosefu wa mvua imeendelea kuwa changamoto kubwa kwa jamii nyingi, hasa katika maeneo yanayotegemea kilimo na ufugaji, hali ambayo inaweza kuathiri usalama wa chakula nchini.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu alete mvua ya  baraka na kuisaidia nchi yetu. Taifa linapitia kipindi kigumu kinachohitaji umoja, hekima na hatua za pamoja kutoka kwa kila upande,” amesema Sheikh Bini.

Katika maombi hayo, viongozi wengine wa dini na jamii akiwemo Rajab Kipkorir Salah na Azizi Ndamwe Wakoli walisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa, mazungumzo na uwajibikaji wa viongozi katika kutatua changamoto zinazowakumba wananchi.

Wakizungumza katika hafla hiyo, viongozi hao walisema masuala kama ukosefu wa mvua, hali ya maisha na changamoto za kijamii yanahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali, viongozi wa dini na wananchi.

Mbali na changamoto ya mvua, maimamu hao pia wamezungumzia migogoro inayoshuhudiwa katika baadhi ya shule nchini, wakipendekeza kuundwa kwa jopo huru litakalochunguza chanzo cha migomo ya wanafunzi na kutoa mapendekezo ya suluhu ya kudumu.

Kwa mujibu wa Sheikh Abubakar Bini, tatizo la migomo shuleni linahitaji kushughulikiwa kwa kuangalia sababu za msingi badala ya kutegemea hatua za muda mfupi pekee.

“Migogoro katika taasisi za elimu inahitaji uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo chake na kuweka mikakati itakayosaidia kuzuia matukio kama haya kujirudia,” alisema.

Katika masuala ya usalama, viongozi hao wa kidini wameitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya maafisa wa polisi wanaodaiwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano, wakisema uwajibikaji ni muhimu katika kulinda imani ya wananchi kwa taasisi za usalama.

Pia wametoa wito kwa viongozi wakuu wa usalama nchini kuwajibika kutokana na kile walichokitaja kuwa ni kushindwa kudhibiti matukio ya utovu wa usalama katika baadhi ya maeneo.

Maimamu hao wamesema fidia iliyotangazwa kwa baadhi ya waathiriwa wa matukio ya vurugu haitoshi, wakitaka hatua zaidi zichukuliwe ili kuhakikisha haki inapatikana kwa walioathirika.

Maombi haya yanafanyika wiki kadhaa baada ya viongozi wa kitaifa kuungana katika Maadhimisho ya Maombi ya Kitaifa yaliyofanyika jijini Nairobi tarehe 28 Mei, hafla iliyowaleta pamoja viongozi wa serikali, wabunge na viongozi wa dini kwa lengo la kuombea umoja, maridhiano na mustakabali wa taifa.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *