Maafisa Wawili wa Polisi Wahukumiwa Miaka 35 Jela kwa Kumuua Mshukiwa na Kutupa Mwili Mtoni

0

Kesi hiyo ilisikilizwa kwa muda wa miaka mitatu ambapo jumla ya mashahidi 21 walitoa ushahidi, wakiwemo wazazi wa marehemu, Safani Malongo na Agnes Ambale, waliosikitishwa na tukio hilo na kuomba haki itendeke.

Picha/Hisani.

Na George Misati

Maafisa wawili wa polisi wamehukumiwa kifungo cha miaka 35 jela kila mmoja kwa kumuua mshukiwa aliyekuwa rumande na kutupa mwili wake kwenye Mto Nzoia, tukio lililotokea mwaka 2020, Mahakama Kuu ya Eldoret iliamua Jumanne, Julai 29, 2025.

Godwine Sirengo Wekesa na Emmanuel Wafula Viambaka walihukumiwa na Jaji Reuben Nyakundi baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Dennis Lusava ndani ya Kituo cha Polisi cha Mburruru kilichopo katika Kaunti Ndogo ya Likuyani, Kaunti ya Kakamega.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, maafisa hao walimkamata Lusava kwa madai ya kutovaa barakoa, wakamfunga pingu kwenye dirisha la kituo hicho cha polisi na kumtesa kwa vipigo vikali hadi alipofariki. Baadaye, waliufunga mwili wake kwenye gunia na kuutupa katika Mto Nzoia, karibu na mpaka wa kaunti za Bungoma na Kakamega.

Akisoma hukumu, Jaji Nyakundi alisema maafisa hao walivunja sheria kwa kutumia mamlaka yao vibaya na kusaliti dhamana waliyopewa ya kulinda raia. “Vitendo hivi ni mfano wa uhalifu uliokithiri unaohitaji adhabu kali kama funzo kwa wengine wanaovunja haki za binadamu,” alisema jaji huyo.

Kesi hiyo ilisikilizwa kwa muda wa miaka mitatu ambapo jumla ya mashahidi 21 walitoa ushahidi, wakiwemo wazazi wa marehemu, Safani Malongo na Agnes Ambale, waliosikitishwa na tukio hilo na kuomba haki itendeke.

Hukumu hiyo imepongezwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, yakiitaja kama hatua muhimu katika kudhibiti ukatili wa polisi na kurejesha imani ya wananchi katika mfumo wa sheria.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *