Wakazi wa Uasin Gishu Wapinga Mafunzo ya Silaha kwa Vijana wa NYS, Wadai Yatishia Usalama wa Nchi

0

“Tunaomba Rais, iwapo tangazo lake litatekelezwa, basi ingekuwa vyema kama vijana hao wakichukuliwa moja kwa moja katika vikosi vya usalama ili kuwaepusha kujiingiza katika uhalifu,”

88th National Youth Service (NYS) Recruits Pass-Out Parade Held in Gilgil, Nakuru County

Baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Uasin Gishu, wakiongozwa na mfanyabiashara maarufu Hassan Kosgey na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Madhehebu ya Kidini, Sheikh Abubakar Bini, wamekosoa vikali tangazo la Rais William Ruto la kuwataka makurutu wa Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kufundishwa namna ya kutumia silaha. Viongozi hao wanasema kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha changamoto kubwa za kiusalama nchini iwapo haitazingatiwa kwa makini.

Hassan Kosgey alisema, “Tunafikiria kuwa mafunzo ya kutumia silaha kwa vijana wa NYS yanaweza kuwa na athari mbaya iwapo vijana hao hawataweza kupata ajira mara baada ya mafunzo. ‘Iwapo vijana hao hawatapata ajira, kuna uwezekano mkubwa wa ongezeko la visa vya uhalifu unaohusisha matumizi ya silaha,’” aliongeza. Alisisitiza umuhimu wa kuajiri moja kwa moja vijana wanaopitia mafunzo hayo katika vikosi vya usalama kama vile polisi, idara ya magereza, na hata jeshi. “Tunaomba Rais, iwapo tangazo lake litatekelezwa, basi ingekuwa vyema kama vijana hao wakichukuliwa moja kwa moja katika vikosi vya usalama ili kuwaepusha kujiingiza katika uhalifu,” alisema Kosgey.

Sheikh Abubakar Bini, kwa upande wake, alitoa wito kwa serikali kuweka mipango na mifumo madhubuti itakayohakikisha kuwa vijana wanaopata mafunzo ya silaha kutoka NYS hawatakuwa tishio kwa usalama wa taifa. Alieleza wasiwasi wake kuwa, “Bila mipango thabiti, vijana waliopata mafunzo ya silaha wanaweza kuwa chanzo cha matukio ya uhalifu nchini, kama ilivyoonekana katika mataifa mengine yaliyoendelea, ambapo vijana wanaojua kutumia silaha wamekuwa wakitumia ujuzi huo vibaya.”

Sheikh Bini pia alihimiza serikali kufanya uchunguzi wa kina na ufuatiliaji wa wale wote wanaopitia mafunzo hayo ili kuhakikisha kuwa mafunzo hayo hayaishii kuwa na athari mbaya kwa jamii. “Ni muhimu kuwa na mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa vijana hawa wanatumia mafunzo yao kwa manufaa ya taifa, na si vinginevyo,” aliongeza.

Tangazo la Rais Ruto lilitolewa jana wakati wa hafla ya kufuzu kwa makurutu wa NYS katika kituo cha mafunzo cha Gilgil, ambapo aliagiza kusajiliwa kwa makurutu wengine zaidi ya elfu ishirini mwaka ujao. Rais Ruto alisisitiza kuwa mafunzo haya ya kutumia silaha yatawasaidia vijana kuwa tayari kujitolea kulinda taifa katika hali yoyote ile ya hatari. “Tunahitaji vijana wenye ujuzi na ujasiri wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zozote za kiusalama zinazoweza kutokea,” alisema Rais Ruto.

Hata hivyo, viongozi hao wameeleza kuwa ingawa nia ya Rais Ruto inaweza kuwa nzuri, utekelezaji wa mpango huo lazima uzingatie maslahi mapana ya usalama wa nchi na utulivu wa kijamii. Wamehimiza ushirikiano kati ya serikali na wadau wengine katika sekta ya usalama ili kuhakikisha kuwa mafunzo haya yanatoa matokeo chanya na hayawi chanzo cha matatizo mapya ya kiusalama nchini.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *