VIONGOZI WA KIISLAMU WAMTAKA AG KUHARAKISHA UTEUZI WA MAKAMISHNA WA WAKFU
Zoezi hili lilikamilika zaidi ya majuma mawili yaliyopita, na tunaona kuna haja ya uchapishaji kufanywa. Tunaomba pia wanasiasa wasiweze kuingiza siasa zao kwenye zoezi hili,” alisema Sheikh Bini.
Sheikh Abubakar Bini . File Photo
By James Gitaka
Viongozi wa Kiislamu katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wanamtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dorcas Oduor, kuchapisha haraka majina ya makamishna wanane waliopendekezwa kuongoza Tume ya Wakfu nchini Kenya.
Wakizungumza na wanahabari jijini Eldoret, Sheikh Abubakar Bini na Imam Abdulaziz Mohammed wamesema jopo lililohusika na mchakato wa uteuzi tayari limekamilisha kazi yake na kuwasilisha majina ya makamishna hao, lakini uchapishaji rasmi bado unasubiriwa.
Sheikh Bini amesema hatua hiyo inapaswa kukamilishwa ili makamishna waanze kutekeleza majukumu yao rasmi.
“Tunamwomba Mwanasheria Mkuu achapishe kwa dharura majina ya makamishna hao ili waweze kuanza majukumu yao rasmi. Zoezi hili lilikamilika zaidi ya majuma mawili yaliyopita, na tunaona kuna haja ya uchapishaji kufanywa. Tunaomba pia wanasiasa wasiweze kuingiza siasa zao kwenye zoezi hili,” alisema Sheikh Bini.
Kwa upande wake, Imam Abdulaziz Mohammed amesema kukamilishwa kwa mchakato huo ni muhimu kwa sababu mali za wakfu zinasaidia Waislamu wengi wasiojiweza.
“Mali ya wakfu husaidia Waislamu wengi wasiojiweza, na hivyo kuna haja ya zoezi hili kukamilishwa kwa wepesi ili makamishna hao waweze si tu kulinda mali za wakfu, bali pia kusaidia Waislamu wengi wanaotegemea wakfu,” alisema Imam Abdulaziz.
Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mali za wakfu zinalindwa na kusimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji ili manufaa yake yawafikie walengwa.
Tume ya Wakfu ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakfu ya mwaka 2022, inayoweka mfumo wa kisheria wa kusimamia na kulinda mali zinazotolewa kwa madhumuni maalumu ya kidini na kijamii.
Viongozi hao sasa wanaitaka serikali kukamilisha hatua zilizosalia za uteuzi ili tume hiyo iweze kuanza kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya jamii ya Kiislamu nchini.
Mchakato huo ulianza kwa kutangazwa kwa nafasi za uteuzi na kupokea maombi 148. Kati ya waombaji hao, 35 waliorodheshwa kwa mahojiano yaliyofanyika kati ya Septemba 14 na 18, 2026. Jopo pia lilipokea maoni 39 yaliyoandikwa kutoka kwa wanajamii wa Kiislamu kuhusu wagombea walioorodheshwa.
Makamishna wanane waliopendekezwa wanajumuisha mwanazuoni wa Kiislamu, mjasiriamali au mfanyabiashara mashuhuri, pamoja na wataalamu sita wenye ujuzi katika nyanja mbalimbali.
Tume hiyo ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakfu ya mwaka 2022, inayoweka mfumo wa kisheria wa kusajili, kusimamia na kulinda mali za wakfu nchini. Majukumu yake yanajumuisha kusimamia matumizi ya mali hizo, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha zinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa. Kenya Law — Waqf Act, 2022
Kwa mujibu wa kifungu cha saba cha sheria hiyo, jopo la uteuzi linapaswa kutangaza nafasi, kuorodhesha waombaji wanaostahili, kufanya mahojiano, kupokea maoni ya Waislamu kuhusu wagombea na kuwasilisha majina ya waliofaulu kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya uteuzi.
Viongozi hao wa Kiislamu sasa wanataka hatua iliyosalia ikamilishwe bila ucheleweshaji , wakisema kuanzishwa kikamilifu kwa tume hiyo kutaimarisha usimamizi wa mali za wakfu na kulinda maslahi ya Waislamu kote nchini.
