Viongozi wa Kiislamu North Rift Waonya Kuhusu Hatari ya Makundi ya Kihalifu
Baadhi ya Viongozi wa Kiislamu Eldoret wahutubia wanahabari.
Na James Gitaka
Viongozi wa Kiislamu katika eneo la North Rift wameonya kuhusu ongezeko la makundi ya kihalifu yanayodaiwa kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kuvuruga mikutano ya kisiasa, wakisema hali hiyo inaweza kuwa tishio kwa usalama wa nchi hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Viongozi hao wametaka Serikali, kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani na vyombo vya usalama, kuchukua hatua za mapema dhidi ya makundi hayo na kuhakikisha vijana hawatumiwi kama chombo cha vurugu za kisiasa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Maulid jijini Eldoret, Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Kenya (CIPK) Kanda ya North Rift, Sheikh Abubakar Bini, alisema amani inapaswa kulindwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Serikali inapaswa kuchukua hatua mapema dhidi ya makundi yanayotumiwa kuvuruga amani. Hatutaki kuona vijana wakitumiwa kisiasa leo halafu kesho makundi hayo yakageuka kuwa tishio kwa usalama wa wananchi,” alisema Sheikh Bini.
Fatih Ahmed, mmoja wa viongozi walioshiriki maadhimisho hayo, alisema matumizi ya makundi ya wahuni katika shughuli za kisiasa yanaweza kuacha mtandao wa uhalifu ambao ni vigumu kudhibiti baada ya uchaguzi.
“Tumewaona wanasiasa kutoka mirengo mbalimbali wakizungukwa na makundi ya vijana wanaotuhumiwa kufanya vurugu. Tunaiomba Wizara ya Usalama wa Ndani kuyachunguza na kuyakabili makundi haya mapema kwa sababu baada ya uchaguzi yanaweza kuwa hatari kwa Wakenya na hata kuhusishwa na mitandao mingine ya kihalifu,” alisema Ahmed.
Wito huo unajiri wakati wasiwasi kuhusu siasa za wahuni zimeongezeka nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.
Taarifa ya hivi karibuni ya Human Rights Watch ilisema makundi ya watu wanaodaiwa kuwa na uhusiano na siasa yamehusishwa na mashambulizi dhidi ya mikutano ya kisiasa na kiraia katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha kabla ya uchaguzi. Shirika hilo limeitaka Serikali kuhakikisha uchunguzi wa haraka na wa uwazi pamoja na kuwawajibisha waliohusika.
Mamlaka ya Kusimamia Utendaji wa Polisi nchini (IPOA) pia imeonya kuhusu wahuni kuhusishwa na mafisa wa usalama na kusema ni tishio na kutaka hatua za kiintelijensia pamoja na ushirikiano wa jamii na uwajibikaji wa wahusika ili kulikomesha.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amekuwa akiwataka wanasiasa kuacha kuajiri au kutumia vijana kusababisha vurugu katika mikutano ya kisiasa, akisema vyombo vya usalama vinaimarisha operesheni za kuwatambua na kuwakamata wanaopanga kuvuruga amani.
Viongozi wa Kiislamu waomba uchaguzi wa haki
Viongozi hao pia wameitaka Serikali kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2027 unaendeshwa kwa njia huru, ya haki na yenye kuwapa Wakenya nafasi ya kuchagua viongozi bila vitisho au vurugu.
Sheikh Bini alisema uchaguzi wa amani unahitaji viongozi wa kisiasa kuheshimu sheria na kuwaepuka vijana wanaoweza kutumiwa kuwazima wapinzani wao kisiasa.
“Tunaiomba Serikali kuhakikisha kila Mkenya anapata nafasi ya kushiriki uchaguzi kwa uhuru na bila vitisho. Wanasiasa wanapaswa kushindana kwa sera na hoja badala ya kutumia vijana kuvuruga mikutano ya wapinzani wao,” alisema.
Wito huo unaungwa mkono na viongozi wengine wa kidini na wazee wa North Rift ambao hivi karibuni walikutana Eldoret na kuwataka wanasiasa kuacha lugha ya uchochezi, ukabila na chuki wanapoanza kampeni za kuelekea uchaguzi wa 2027.
Maulid yaunganishwa na maombi kwa waathiriwa wa mkasa wa tanker Eldoret
Katika hafla hiyo, viongozi na waumini wa Kiislamu pia waliendesha ibada maalum kuwaombea waliopoteza maisha na waliojeruhiwa katika mkasa wa moto uliotokea kwenye barabara ya Eldoret-Webuye karibu na Shule ya Upili ya Paul Boit.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 17, 2026, baada ya lori la mafuta kupinduka katika eneo la Kapkong karibu na Paul Boit. Baadhi ya watu waliripotiwa kufika eneo la ajali na kuanza kuchota mafuta yaliyokuwa yakivuja kabla ya moto mkubwa kuzuka.
Kwa mujibu wa Moi Teaching and Referral Hospital (MTRH), watu 22 walikuwa wamepokelewa hospitalini kufuatia mkasa huo, huku 10 wakiwa katika hali mbaya na kupata majeraha makubwa ya kuungua yaliyofikia kati ya asilimia 40 na 50 ya miili yao. Hospitali ilisema watu watatu walikuwa wamefariki kufikia Septemba 18.
Ripoti zilionyesha kuwa waathiriwa 11 kati ya 23 waliokuwa wakipokea matibabu walikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kutokana na majeraha makubwa ya moto.
Sheikh Bini alikosoa tabia ya baadhi ya wananchi kukimbilia kuchota mafuta baada ya ajali za malori ya mafuta, akisema tamaa ya kupata mafuta inaweza kusababisha vifo na majeraha makubwa.
“Ni jambo la kukosa utu kabisa kwamba badala ya wananchi kukimbilia kusaidia kuokoa maisha baada ya ajali, baadhi yao hukimbilia kuchota mafuta. Hii ni hatari sana kwa sababu mafuta yanapovuja yanaweza kusababisha moto na mlipuko wakati wowote,” alisema Sheikh Bini.
Aliwataka wananchi kuacha kujihatarisha katika maeneo ya ajali na badala yake kutoa nafasi kwa polisi, wazima moto, wahudumu wa afya na timu za uokoaji kufanya kazi.
“Tunawaombea shufaa wote walioathirika katika mkasa huu na tunatoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Somo kubwa tunalopaswa kulipata ni kwamba maisha ya binadamu yana thamani kuliko mafuta yanayoweza kuchotwa kutoka kwenye tanker iliyopata ajali,” alisema.
Mamlaka za usalama pia zimekuwa zikionya wananchi dhidi ya kukaribia malori ya mafuta yaliyopata ajali kutokana na hatari ya moto na milipuko.
Vijana watakiwa kukataa kutumiwa kisiasa
Vijana waliohudhuria maadhimisho hayo walisema hawatakubali kutumiwa na wanasiasa kufanya vurugu, wakisema jukumu lao ni kushiriki katika siasa kwa njia ya amani na kuwachagua viongozi kwa kuzingatia sera na utendakazi wao.
Ali Mohammed, mmoja wa vijana walioshiriki hafla hiyo, aliwataka vijana wengine kote nchini kukataa vishawishi vya kisiasa vinavyoweza kuwapeleka katika uhalifu.
“Vijana hatutaki kutumiwa kama vyombo vya vurugu. Tunapaswa kutumia kura zetu kuchagua viongozi kulingana na sera, maono na uwezo wao wa kuwatumikia wananchi,” alisema Mohammed.
Alisema vijana wana nafasi muhimu ya kulinda amani wakati wa uchaguzi badala ya kuwa sehemu ya makundi yanayoweza kuvuruga mikutano au kushambulia wapinzani wa kisiasa.
“Tofauti za kisiasa zisigeuke kuwa chuki kati ya vijana. Tunaweza kuwa na mitazamo tofauti lakini bado tukawa majirani, marafiki na Wakenya wenzetu baada ya uchaguzi,” alisema.
