Kosachei Waapa Kutwaa Ushindi Katika Mashindano ya Voliboli, Eldoret
Kwa upande wao, wanafunzi kupitia kwa nahodha wao Mercy Jerop,wamesema kuwa watajikakamua mazoezini na hata michezo yenyewe itakapoanza.
Timu ya voliboli ya wasichana kutoka shule ya Msingi ya Kosachei. Picha/Kosachei Journalism Club.
Na Wesley Kiplimo
Timu ya voliboli ya wasichana wa shule ya msingi ya Kosachei imezidisha mazoezi yao katika kujitayarisha kwa mashindano ya voliboli yatakayofanyika jijini Eldoret.
Mashindano hayo yanayofadhiliwa na Oliva Kipchumba Karori, mkuu wa kitengo cha sheria katika ofisi ya Rais William Ruto yatafanyika kuanzia tarehe kumi na tatu hadi tarehe kumi na tano Disemba.
Wachezaji wa shule ya msingi ya kosachei wanafanya maandalizi chini ya mkufunzi wao Cheruiyot Jackson.
Kulingana na mkufunzi Cheruiyot, kikosi chake kitaendelea na mazoezi yao shuleni hadi tarehe kumi na moja Disemba, siku moja kabla ya mashindano hayo kungo’a nanga katika chuo cha anuwai cha Eldoret.
“Wasichana wangu tayari wamerudi kambini baada ya kuenda likizoni. Hii ni kwa sababu tunajiandaa kwa michezo itakayofanyika Eldoret Polytechnic. Warembo wangu wote wamerudi na nashukuru Mungu kwamba kila mmoja yuko sawa kiafya na tayari,’’ alisema Cheruiyot.
Kwa upande wao, wanafunzi kupitia kwa nahodha wao Mercy Jerop,wamesema kuwa watajikakamua mazoezini na hata michezo yenyewe itakapoanza.
Wameitambua shule ya msingi ya Soin kama tishio lao kwenye mashindano hayo. Hata hivyo, wana imani watawabwaga.
“Sisi tumefurahi kurudi kambini kwa mazoezi. Kila mwanafunzi ana furaha kwa sababu ya mechi hii kubwa ambayo itatusaidia kukuza mazozi yetu na hata kuonyesha nchi nzima kwamba sisi pia ni Malkia chipukizi,’’ alisema Mercy.
“Tishio letu tu kundini ni wasichana wa shule ya msingi ya Soin waliotuchapa kwenye michezo ya shule za msingi lakini tulirekebisha makosa yetu na tuko na imani kuwa tutawabwaga mara hii,’’ aliongezea msichana huyu wa gredi ya nane kaskazini.
Michezo hiyo itajumuisha mashindano baina ya shule za msingi, shule za upili, pamoja na timu tajika ikiwemo ile ya maafisa wa GSU, Walinzi wa Magereza (Kenya Prisons), Benki ya Equity, Wafanyikazi wa kampuni ya KPA na nyinginezo nyingi.
Shule za msingi ambazo tayari ziko kwa ratiba ni Pamoja na Kosachei, Soin, Kaliwa, Cheptiki miongoni mwa timu zingine.
