FAMILIA YA MWANAJESHI WA KENYA ALIYETEKWA NA WANAMGAMBO WA ALSHABAB YAWAOMBA SERIKALI KUMREJESHA NYUMBANI BAADA YA MIAKA MINANE
“Wanamgambo wa Al-Shabaab wamesema wako tayari kuzungumza na serikali ya Kenya kuhusu kumwachilia Issa huru”

Katrina Abdullahi Issa akiwa nyumbani, ameshikilia picha ya baba yake, Abdullahi Issa Mohamed, mwanajeshi wa Kenya aliyetekwa na wanamgambo wa Al-Shabaab miaka minane iliyopita,
Familia ya Abdullahi Issa Mohamed, mwanajeshi wa Kenya mwenye umri wa miaka 61, aliyezingirwa na hatma isiyoeleweka kwa muda wa miaka minane baada ya kutekwa na wanamgambo wa Al-Shabaab mnamo Januari 15, 2016, sasa wanaomba serikali ya Kenya kuongeza juhudi za kumrejesha nyumbani. Issa, ambaye alitekwa nyara wakati wa shambulizi kwenye kambi ya El-Adde nchini Somalia, alikuwa sehemu ya kikosi cha tisa cha maafisa wa ulinzi wa Kenya kilichokuwa kimeingia nchini humo mnamo Januari 1, 2016, katika juhudi za kurejesha amani na utulivu.
Katika video ya kusikitisha iliyosambazwa mitandaoni hivi karibuni, Issa alionekana akitoa wito wa msaada wa kuunganishwa na familia yake. Tukio hili limezua hisia mchanganyiko miongoni mwa familia yake, majirani, na wakazi wa eneo lao, huku wengi wakionesha furaha kwa kugundua kwamba Issa bado yuko hai, lakini pia huzuni na maumivu kwa mateso anayokabiliana nayo akiwa mateka.
Historia ya Uingiliaji wa Kenya Somalia
Mnamo mwaka 2011, Kenya ilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab kwa jina “Operation Linda Nchi.” Operesheni hiyo ilikuwa na lengo la kuzuia wanamgambo hao kushambulia maeneo ya Kenya na kuimarisha usalama mpakani. Mwaka mmoja baadaye, mnamo 2012, Kenya iliungana rasmi na African Union Mission to Somalia (AMISOM), hatua iliyoongeza ushirikiano wa kikanda katika juhudi za kurejesha amani nchini Somalia. Tangu wakati huo, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limekuwa likidhibiti sehemu kubwa ya eneo la Kusini mwa Somalia, hasa katika Mkoa wa Gedo, kwa lengo la kuzuia wanamgambo wa Al-Shabaab na kuimarisha uthabiti wa kisiasa na kiusalama nchini Somalia.
Hata hivyo, juhudi hizi za kijeshi zimekuja na changamoto kubwa, ikiwemo maisha ya wanajeshi kupotea, wengine kutekwa, na familia zao kuteseka huku wakisubiri matumaini ya wapendwa wao kurudi nyumbani salama. Tukio la Abdullahi Issa Mohamed ni mojawapo ya mifano hai ya changamoto hizi, ambapo miaka minane baada ya kutekwa kwake, familia yake bado inaishi katika maumivu na matarajio.
Familia Yamlilia Mpendwa Wao
Kwa mujibu wa Katrina Abdullahi Issa, mtoto wa kwanza wa Issa, familia yao ililazimika kufanya mazishi ya kiishara baada ya miaka sita ya maombolezo kufuatia kukatika kwa mawasiliano na baba yao. Akiwa na machozi, Katrina alielezea maumivu yao ya kihisia lakini pia matumaini ya kuona baba yao akirejea nyumbani. Alisema:

“Kwa baba yangu, kama Allah amekuweka hai muda wote huu, usichoke, tunakuombea. Karibu utakuja nyumbani, inshaAllah. Sikujua maisha yako yakiwa mateka yako namna gani, lakini utakuja nyumbani. Tutakuandalia vyakula unavyovipenda na tukuchunge.”
Kwa mujibu wa Katrina, familia imekuwa ikivumilia mateso makubwa ya kisaikolojia tangu baba yao alipotoweka. Walipoteza matumaini na kufikia hatua ya kufanya mazishi ya kimya kimya, lakini sasa, baada ya video ya baba yao kujitokeza, wanashikilia tena imani kwamba bado anaweza kurudi nyumbani salama.
Majirani na Wakazi Waonyesha Furaha na Matarajio
Majirani wa familia na wakazi wa eneo la maili nne viungani mwa mji wa Eldoret hawakuficha furaha yao baada ya kusikia kwamba Issa bado yuko hai. Wengi walikusanyika katika mkutano wa maombi na kuunga mkono familia huku wakitoa wito kwa serikali kuingilia kati haraka.
“Tunaomba serikali ifanye juhudi za dhati kuzungumza na Al-Shabaab kwa ajili ya kumuokoa Issa na kuhakikisha anaunganishwa na familia yake,” alisema mmoja wa majirani.

Wakazi wengine walieleza hisia zao kuhusu kujitolea kwa wanajeshi wa Kenya kama Issa, ambao wamepoteza maisha yao au kuteseka kwa ajili ya nchi.
“Wanajeshi wetu wanapigana kwa ajili ya usalama wetu. Tunatoa heshima kwao, lakini pia tunawaomba viongozi wa serikali wahakikishe wanapewa msaada wa kurudi kwa familia zao wakati wanapokumbwa na changamoto kama hizi,”alisema mkazi mmoja wa eneo hilo.
Wito wa Viongozi wa Dini
Katika hafla ya maombi iliyoandaliwa na familia, viongozi wa kidini walihimiza serikali kutumia uwezo wake wote kuhakikisha Issa anarudi salama.
Sheikh Abdikadir Mallim, akizungumza kwa hisia, alisema:
“Tunamuomba Rais na Waziri wake wa Ulinzi waingilie kati. Issa arejeshwe nyumbani. Amehangaika akitetea na kulinda nchi ya Kenya. Ni haki yake kurejea kwa familia yake. Serikali inapaswa kuchukua jukumu hili haraka.”

Kwa upande wake, Sheikh Ali Adan alitoa wito wa dhati kwa Rais William Ruto, akisema:
“Kwa Rais wetu, tunakuomba utumie nguvu zako zote kuhakikisha askari huyu anarudi nyumbani chini ya wiki moja. Unao uwezo wa kufanya hivyo. Tunapongeza jeshi letu kwa kujitoa mhanga ili tupate amani, lakini tunawaomba pia watoto na wake wa wanajeshi hawa wasiachwe yatima. Inawezekana Issa arejeshwa nyumbani salama, inshaAllah.”
Sheikh Abubakr Bini, ambaye aliongoza dua hiyo, alisisitiza umuhimu wa kuwa na subira na kuendelea kuomba msaada wa Mungu, huku akitoa wito kwa viongozi wa serikali kuonyesha huruma kwa familia zinazoteseka kwa sababu ya hali kama hizi.
“Hili ni suala ambalo linaumiza roho. Tunawaomba viongozi wetu walione hili kwa jicho la huruma. Tunaendelea kumwomba Allah amlete Issa salama,” alisema Sheikh Bini.
Al-Shabaab Wako Tayari Kujadiliana
Kwa mujibu wa familia, wanamgambo wa Al-Shabaab wamesema wako tayari kuzungumza na serikali ya Kenya kuhusu kumwachilia Issa huru. Familia inatoa wito kwa viongozi wa serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mazungumzo haya yanakuwa na matokeo chanya.
“Hatuna mawasiliano ya moja kwa moja na Al-Shabaab, lakini tumepata habari kuwa wako tayari kuzungumza. Hii ni fursa ya kipekee ambayo serikali haipaswi kupoteza,” alisema mmoja wa wanafamilia.
Wanajeshi Wengine Bado Wanazuiliwa
Mbali na Issa, inaripotiwa kwamba kuna maafisa wengine sita wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) ambao bado wanashikiliwa na wanamgambo hao. Familia ya Issa na wananchi wana matumaini kwamba juhudi za kumwokoa Issa zinaweza kuwa mwanzo wa mchakato wa kuwaokoa pia wanajeshi wengine waliotekwa.