Maimamu Watishia Maandamano Dhidi ya SUPKEM, Wakidai Ufisadi na Udhalimu Katika Usimamizi wa Mahujaji
“Tumechoshwa na ubabe na ufisadi unaoendelea ndani ya SUPKEM”
Maimamu kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini wakihutubia wanahabari kuhusu madai ya ufisadi na ukosefu wa uwajibikaji ndani ya Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM), wametoa wito wa mageuzi ya haraka ili kulinda haki za mahujaji/James Gitaka
Na James Gitaka
Mzozo unaoendelea kuhusu usimamizi wa Hajj nchini Kenya umezidi kuchacha baada ya maimamu kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa kutangaza mpango wa kuandaa maandamano makubwa dhidi ya Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM) na kupeleka lalalama hizo hadi Ubalozi wa Saudi Arabia jijini Nairobi.
Wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini na Sheikh Mohammed Abdulaziz, viongozi hao wa Kiislamu wameshtumu SUPKEM kwa kile walichokitaja kama “ufujaji wa mamilioni ya pesa za mahujaji, ukosefu wa uwajibikaji na udhalimu wa wazi dhidi ya watoa huduma halali wa Hajj na Umrah.”
“Tumechoshwa na ubabe na ufisadi unaoendelea ndani ya SUPKEM. Wamezuia maajenti 16 waliokuwa wakihudumu kwa uadilifu, ikiwemo Al Saadah & Umrah Agency, kwa sababu tu walihoji mazingira mabovu ya mahujaji mwaka jana,” alisema Sheikh Bini.
Maimamu hao wanasema maajenti waliosimamishwa walikuwa miongoni mwa wale walioibua malalamiko kuhusu mazingira duni waliyokumbana nayo mahujaji wa Kenya nchini Saudi Arabia wakati wa Hajj ya 2025. Malalamiko hayo yalihusu makazi duni, uhaba wa chakula, na kutengwa kwa mahujaji katika maeneo ya mbali zaidi kuliko yale waliyolipia.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mahujaji walilipia takriban USD 1,300 (karibu KSh 170,000) kwa huduma ikiwemo malazi, chakula, usafiri, na ada ya SUPKEM ya USD 100, lakini walipata huduma duni na kukaa katika “zone 6,” zaidi ya kilomita 14 kutoka maeneo ya ibada, tofauti na “zone 4” waliyolipia.
“Ni dhuluma ya kidini kuwatwisha mahujaji mzigo mkubwa wa kifedha halafu wawape huduma zisizofaa. Badala ya kuwajibika, SUPKEM imeamua kulipiza kisasi kwa kufunga huduma za maajenti waliolalamika,” aliongeza Sheikh Abdulaziz.
Maajenti walioathiriwa, wakiwemo wawakilishi wa Al Saadah & Umrah Agency—pekee kutoka Bonde la Ufa—wameshatangaza kuwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua ya kufutiwa huduma na baraza hilo. Kesi hiyo tayari imepokelewa katika Mahakama Kuu ya Nairobi.
Kulingana na ripoti kutoka mashirika ya habari kama Eastleigh Voice na The Star, maajenti wa Hajj kutoka maeneo ya Pwani pia wamekosoa SUPKEM kwa kuendesha mipango ya mahujaji kwa njia ya kifisadi bila ushauri wa wadau muhimu. Mwaka huu pekee, idadi ya mahujaji wanaosafirishwa kupitia baadhi ya maajenti hao imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 80.
“Wametubagua. Hakuna uwazi wala ushirikishwaji. Walifanya mikutano ya kupanga Hajj ya 2026 na maajenti wachache waliowachagua wao binafsi,” alisema Sheikh Abdulkadir Al-Ubeidy kutoka Mombasa.
Maimamu sasa wanamtaka Waziri wa Masuala ya Kigeni, Musalia Mudavadi, kuingilia kati mzozo huu na kuanzisha mchakato wa mageuzi ya kina ndani ya SUPKEM. Wanapendekeza kuundwa kwa jopo jumuishi linaloshirikisha mashirika mengine ya Kiislamu kama CIPK ili kuhakikisha maelfu ya Waislamu nchini wanapata fursa ya kutekeleza nguzo ya tano ya Uislamu bila kunyanyaswa.
“Tunataka baraza jipya la kushughulikia haki za mahujaji na kuweka uwazi katika usimamizi wa fedha na huduma. Ikiwa hili halitafanyika, basi tutashiriki maandamano ya kitaifa hadi haki ipatikane,” alihitimisha Sheikh Bini.
SUPKEM bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu madai hayo, lakini vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa baraza hilo linapanga kuitisha mkutano wa dharura kujibu lawama hizo.
