Wanawake Watoa Wito Wa Haki na Mazungumzo Kufuatia Taharuki Inayoongezeka
“Serikali inapaswa kutangaza Siku ya Kitaifa ya Maombolezo na Tafakari, kama ishara ya mwanzo mpya wa maridhiano na mwelekeo wa kitaifa wa pamoja”Kina Mama wa Taifa na Mabalozi wa Amani wa Kike Nchini Kenya
Mary Njoki, Uasin Gishu Coordinator of Echo Network Africa Foundation (ENAF), Image: Courtesy of Hubz Media
Kina Mama wa Taifa na Mabalozi wa Amani wa Kike Nchini Kenya wametoa tamko la pamoja wakilitaka taifa kuchukua mwelekeo wa haki, maridhiano, na uponyaji wa kitaifa, wakati ambapo nchi inatikiswa na mivutano ya kisiasa, migawanyiko ya kijamii na athari za maandamano yaliyotokana na Mswada wa Fedha wa 2024.
Wakiongozwa na Mary Njoki, Mshirikishi wa Echo Network Africa Foundation (ENAF) katika kaunti ya Uasin Gishu, kina mama hao wamesema taifa liko katika njia panda na lina kila sababu ya kusitisha mwelekeo wa migawanyiko na badala yake kujenga umoja kupitia mazungumzo ya kweli na uongozi wa kimaadili.
“Kama wanawake tunaamini katika uwezo wa jamii kupona kupitia majadiliano ya wazi. Sauti za kina mama hazipaswi kupuuzwa, kwani sisi ndio nguzo ya maadili ya taifa. Leo tunasimama kwa niaba ya familia, watoto wetu, na mustakabali wa Kenya,” alisema Mary Njoki.
Kundi hilo limeonesha masikitiko makubwa kufuatia vifo na majeraha yaliyowakumba waandamanaji, yakiwemo mauji ya kikatili ya mwanablogu Albert Ojwang , Boniface Kariuki aliyepoteza fahamu kutokana na majeraha, na Philip Oketch, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta ambaye bado yuko katika hali mahututi.
“Maumivu yetu ni makubwa lakini hamasa yetu ya kudai haki ni ya kudumu. Tunasema wazi kwamba wote waliohusika na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu lazima wawajibishwe ipasavyo,” aliongeza Njoki.
Pamoja na kutoa wito kwa viongozi wa serikali na wananchi kwa ujumla, wametaka Serikali kutangaza Siku ya Kitaifa ya Maombolezo na Tafakari, kama ishara ya mwanzo mpya wa maridhiano na mwelekeo wa kitaifa wa pamoja.
Katika taarifa yao rasmi, walitoa mwito kwa:
-
Vijana wa Gen Z, kuendelea na maandamano kwa njia ya amani na heshima kwa wale waliopoteza maisha;
-
Vyombo vya usalama, kuheshimu haki ya kikatiba ya kuandamana kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 37 ya Katiba;
-
Viongozi wa dini, kusimama kama nguzo ya maombi, maridhiano na mshikamano wa kitaifa;
-
Rais wa Jamhuri ya Kenya, kutekeleza mamlaka yake kwa kuhakikisha vikosi vya usalama vinazingatia sheria na haki;
-
Serikali, kutangaza Siku ya Kitaifa ya Maombolezo na Tafakari kama hatua ya kuanza upya safari ya kujenga Kenya yenye mshikamano, haki na maridhiano.
“Amani si ukimya wa waliokandamizwa, bali ni matokeo ya haki inapotendeka. Sisi hatusimami tu kama waombolezaji, bali kama wajenzi wa taifa jipya lenye mshikamano, maadili na haki kwa wote,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa upande wao, viongozi wa dini ya Kiislamu kutoka Kanda ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini, wamelaani ghasia zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano , huku wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa ili kuzuia mzozo zaidi.
“Tumesikitishwa na matukio ya kuchomwa kwa magari ya polisi na makundi ya watu waliokuwa na mipini wakitishia waandamanaji wanaotekeleza haki yao ya kikatiba. Hii si njia ya kusuluhisha matatizo ya taifa letu,” alisema Sheikh Bini.
Aliendelea kusema kuwa ni muhimu kuanzisha majadiliano ya kweli kati ya serikali na vijana, akisisitiza kuwa viongozi wa dini wako tayari kusimamia mchakato wa maelewano.
“Tunapendekeza kuwepo kwa mazungumzo yanayoongozwa na viongozi wa kidini ili kujenga daraja kati ya vijana na serikali. Njia ya mabavu haitatupeleka mbali—hasa tunapoelekea kipindi cha uchaguzi,” aliongeza.
