Mchango wa Lugha ya Kiswahili katika Maendeleo ya Utamaduni na Mawasiliano: Mafanikio na Changamoto

0

Washikadau mbalimbali wanashabikia Kaunti ya Uasin Gishu kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kusherehekea lugha ya Kiswahili mwakani

Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi kwa kushirikiana na Idara ya Jinsia, Ulinzi wa Kijamii na Utamaduni katika Kaunti ya Uasin Gishu, Ijumaa iliandaa warsha kwa maafisa wa mawasiliano na wanahabari pamoja na wadau wa sekta ya Kiswahili mjini Eldoret.

Warsha hiyo iliyoongozwa na Afisa Mkuu wa Utamaduni Eunice Suter, ililenga kukuza ufahamu wa umuhimu wa lugha ya Kiswahili.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Suter aliwahimiza washiriki na wadau wengine wa Kiswahili kuzingatia umuhimu wa lugha hiyo na kuitumia kikamilifu katika mawasiliano na maisha ya kila siku.

Aidha, alisisitiza kuwa Kiswahili ni sehemu muhimu ya utamaduni wa taifa, ikichangia katika uwiano na maridhiano, hivyo inapaswa kutunzwa na kutumiwa kwa heshima katika maeneo yote.

Wadau pia walichangia wazo la kuweka sera zinazohimiza lugha ya Kiswahili kwa watoto wa chekechea.

Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni katika Kaunti ya Uasin Gishu, Mohamed Haji, ambaye alihudhuria mafunzo hayo, alisisitiza kwamba Kiswahili ni utamaduni wenyewe.

Alitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa kuendeleza na kusambaza matumizi ya Kiswahili katika jamii.

Kwa pamoja, wadau walikubaliana kuendelea kushirikiana katika kukuza lugha ya Kiswahili na kuieneza zaidi ili iweze kustawi na kutambulika kimataifa.

Mafunzo hayo yalikuwa hatua nzuri na msingi wa kuhamasisha matumizi ya Kiswahili na kuifanya lugha hiyo kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya utamaduni na mawasiliano nchini.

Hatua hii inaonyesha jitihada zilizofanywa na serikali katika kukuza na kulinda lugha  ya kiswahili.

Pia, inatarajiwa kwamba serikali itabuni tume ya kitaifa ya Kiswahili ifikapo mwisho wa mwaka huu. Washikadau mbalimbali wanashabikia Kaunti ya Uasin Gishu kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kusherehekea lugha ya Kiswahili, yanayofanyika kila tarehe saba mwezi wa saba.

Hatua hii itaendeleza utambuzi na umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika ngazi ya kitaifa na kukuza uelewa wa pamoja kuhusu utajiri wa lugha ya kiswahili.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *